Wakenya wanapojiandaa kwa mashamrashamra ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2024 na kuuaga mwaka wa 2023, mengi yametarajiwa.
Lakini kabla ya hayo, Wakenya wameona mengi ya kushangaza mwaka wa 2023. Tupate taswira ya mwaka ulivyokuwa kwa muhtasari.
Kuanzia na mashaka ya Shakahola, Wakenya walistajabishwa na maajabu ya muhibiri tata Paul Mackenzie. Kufikia Oktoba 20, takriban miili mia nne ishirini na tisa ilifukuliwa kutoka makaburi ya Shakahola, katika kaunti ya Kilifi.
Mwaka huu pia ulishuhudia rais William Ruto akiwaonya wafisadi wanaorudisha nchi nyuma, kwa kuangusha kampuni za sukari nchini. Rais alinakili kuwa njia yao itakuwa ni: kubadilika, jela au mbinguni na hivyo kaulimbiu ya “mambo ni matatu” kuanzishwa.
Katika sekta ya elimu Wakenya walishuhudia mwanafunzi jasiri aliyewapa msomo gavana na seneta wa Uasin Gishu. Hii ni baada ya mpango wa ufadhili wa masomo ya juu ughaibuni kufeli, kwa kile kilijulikana kuwa ubadhirifu wa fedha zilizotengewa shughuli hiyo.
Mwanafunzi huyo aliwakaanga kwa maneno viongozi wa Uasin Gishu wakiwemo Gavana Jonathan Bii, Naibu wake John Barorot na Seneta Jackson Mandago.
Takriban wanafunzi 125 walikosa kutimiza ndoto zao za kusoma ughaibuni kupitia mpango huo wa ufadhili wa masomo ya kaunti ya Uasin Gishu. Shilingi milioni thelathini na tatu zisijulikane ziliko.

Jared Nyataya | Nation Media Group
Tukisalia katika sekta ya elimu, ni mwaka ulioshuhudia mtihani wa mwisho wa darasa la nane katika mfumo wa 8-4-4. Mtihani huo ulikumbwa na utata baada ya wazazi na walimu kutoa hisia za kuonyesha kutoridhishwa kwao. Matokeo ya wanafunzi wengine, katika somo lingine, yalikuwa sawia katika shule zingine.
Masomo ya chuo kikuu kulichukua mkondo mpya baada ya jopokazi la rais, kupendekeza mfumo mpya wa kufadhili elimu ya juu. Mapendekezo hayo yamepelekea karo ya masomo ya chuo kikuu kupanda na kuwapa changamoto kubwa wanafunzi kutoka familia maskini.
Katika mwaka wa 2023, serikali ya Kenya Kwanza ilitoa mfumo mpya wa kupata senti kutoka kwa Wakenya. Ushuru. Hii ilipelekea Wakenya kumbatiza rais Ruto na kumuita Zakayo.
Mpango wa kuwatoza wale wanaopata mishahara ushuru wa asilimia tatu (3%) ilipatana na pingamizi kuu kutoka kwa Wakenya, na hivyo kupunguzwa hadi asilimia moja nukta tano (1.5%)
Maandamano yaliyoongozwa na mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya Alliance, yalileta madhara mengi zikiwemo kuharibiwa kwa mali ya umma, Nairobi Expresswa ikiwemo. Watu wapatao waliuawa kutokana na risasi, huku wengine wakipigwa na polisi.

Mali ya kibinafsi pia haikusazwa na waandamanaji.
Ubinafsishaji wa mashirika kumi na moja ya umma yalizoa hisia mseto kutoka kwa Wakenya. Mashirika hayo ni pamoja na KICC, Kenya pipeline, na Kenya Cooperative Creameries (KCC). Wakenya wengine waliingia mtandaoni kujieleza, huku wengine wakiwaza ni kwa nini shirika la Kenya Power halikuwa kwenye orodha hiyo.
Hii ilitokana na kuwa na mazoea ya stima kupotea nchini mara kwa mara. Uwanja wa ndege wa kimataifa Jomo Kenyatta (JKIA) pia ukiathirika.
Tukisalia na ya JKIA, video na picha zilisambaa zikionyesha paa zake zikivuja kulipokuwa na mvua.
Ripoti ya tume ya mazungumzo na maridhiano ya kitaifa ilidhihirisha mianya iliyopo katika mrengo wa Azimio baada ya pande moja kujitenga na ripoti hiyo. Hii ni baada ya upande wa serikali kusita kuzungumzia mambo yanayohusu kupunguza gharama ya maisha ya mkenya wa kawaida.
Gharama ya juu ya maisha ilipelekea watu wengi nchini kusherekea Krismasi kwa bajeti. Wengine hawakuenda mashinani kusherehekea na familia zao kama ilivyo ada. Hivyo, usafiri ulipungua kulinganishwa na miaka ya awali.
Katika usafiri msimu huu wa Krismasi tumeshuhudia matukio mengi, ya ajali barabarani huku watu zaidi ya elfu nne wakipoteza maisha yao, mwaka mzima.

Ni tumaini la Wakenya wengi, kuwa mwaka mpya utakuwa wenye mabadiliko makubwa katika maisha yao: Kuanzia kwa uchumi, uongozi wa nchi, ajira na mengi.
0 Comments